Ukosefu fedha wachangia kuzorotesha kilimo nchini
Imeelezwa kuwa tatizo la ukosefu wa uwezeshaji kifedha katika sekta ya kilimo umekuwa ukichangia kuzorotesha maendeleo ya sekta ya kilimo nchini
Tafiti iliyofanywa na taasisi ya masuala ya kiuchumi na kijamii ESRF ya mwaka 2011 imebainisha kuwa sekta ya kilimo imekuwa ikishuka kwa kiasi kikubwa kutokana na upatikanaji hafifu wa masoko, ukosefu mkubwa wa taaluma ya kilimo cha umwagiliaji hali kadhalika uwepo wa miundo mbinu duni ya uzalishaji wa sekta ya kilimo
Akitoa taarifa hiyo mjini Unguja kwa wadau wa sekta ya kilimo kutoka taasisi mbalimbali za serikali, mtafiti mkuu wa masuala ya sekta ya kilimo kutoka taasisi hiyo Dkt Oswald Mashindano amesema tafiti walizoweza kuzifanya katika ukanda wa Kusini,Kaskazini na Mashariki mwa Tanzania umeonyesha dhahiri wakulima wengi wanashindwa kuzalisha kwa kiasi kikubwa kutokana na matatizo mbalimbali yanayowapelekea kushindwa kufikia malengo ya kukiona kilimo ni sekta muhimu katika ukuaji wa maendeleo yao ya kiuchumi hali kadhalika maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Hatahivyo amesema bado ukulima unaofanyika hivi sasa haujaweza kubadilika na kuendelea kutumia Kilimo cha jembe la mkono suala ambalo sekta hiyo inazidi kuporomoka.
Ameongeza kuwa tatizo lingine ambalo linawafanya wakulima wengi kushindwa kusonga mbele ni ukosefu mkubwa wa uwezeshaji wa rasilimali fedha suala ambalo nalo limekuwa ni changamoto kubwa kwa upande wao .
Baadhi ya wadau waliokuwa katika mdahalo huo wa kujadili tafiti hiyo wamesema kuwa umuhimu mkubwa kwa serikali na sekta binafsi kuangalia uwezekano wa kuwawezesha zaidi wakulima kifedha hali kadhalika na upatikanaji wa masoko ndani na nje ya nchi.
Utafiti huo umeonyesha kuwa asilimia sabini hadi themanini ya watu wengi wamo katika sekta ya Kilimo kati ya hao asilimia 86.5 ni wakina mama lakini bado sekta ya Kilimo haijaweza kufikia malengo ya uzalishaji mkubwa.
Kulthum Ali, TBC Zanzibar.
Last Updated ( Friday, 13 September 2013 13:03 )