Chiza akiri udhaifu sekta ya kilimo
Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Injinia Christopher Chiza amekiri kuwepo kwa udhaifu katika sekta ya kilimo na kwa wauzaji wa teknolojia ya zana za kilimo.
Waziri Chiza amesema kuwa hali hiyo inatokana na kutofanya utafiti wa namna ya kuwafanya wakulima kukuza kilimo huku wauzaji wa zana za kilimo za Waziri kiteknolojia wakiendelea kubaki mjini badala ya kuwafikia wakulima walio katika maeneo ya vijijini.
Injinia Chiza ameyasema hayo katika uzinduzi wa maonesho ya kilimo maarufu kama Nane nane,yanayofanyika mkoani Dodoma kitaifa, ambapo pia serikali haina mpango wa kufuta sherehe za maadhimisho ya siku hiyo ya wakulima.
Siku ya kwanza ya maadhimisho hayo waziri Chiza amemwakilisha rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza mapinduzi Dr. Mohamed Shein.
Katika uzinduzi huo Waziri Chiza alitembelea banda la ofisi ya waziri mkuu na baadae akazuru mabanda mengine mbalimbali, na akaonyesha kushangazwa na jinsi mazao yanavyoshamiri katika maonesho huku wakulima wakiendelea kulia na kilimo kisicho na tija, ambapo waziri chiza amelia na watafiti wataalam, na wauzaji wa teknolojia za ukuzaji kilimo.
Pamoja na hayo, wapo baadhi ya wakulima walioitikia wito wa kilimo kwanza na kuendeleza kilimo kupitia mikopo, lakini kinaibuka kikwazo kingine ambacho ni upungufu au ukosefu wa masoko ya mazao.
Naye mwenyekiti wa TASO ambao ndio waandaaji wa maonesho ya nane nane, Engibert Moyo amesema maonesho hayo yamekuwa yakiandaliwa kitaifa lakini hayajawahi kutengewa bajeti ya uendeshaji, lakini pia akaonyesha hofu ya maonesho hayo kughubikwa na starehe zaidi na kupoteza lengo la nanenane.
Maonesho hayo yanatarajiwa kufikia kilele tarehe saba, na sio tarehe nane kama ilivyo kawaida, ili kuwapa wananchi fursa ya kusherehekea siku kuu ya idd elfitri.
Victoria Patrick, TBC Dodoma.
Last Updated ( Friday, 02 August 2013 09:12 )