Watuhumiwa wa ukataji mkono wa albino wafikishwa mahakamani
Watuhumiwa watano wanaodaiwa kushiriki katika kitendo cha kumkata mkono Mlemavu wa ngozi Albino Maria Chambanenje wa kijiji cha Miangalua wilayani Sumbawanga wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu mkazi wilayani Sumbawanga kusomewa mashtaka yao.
Watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani baada ya uchunguzi wa jeshi la polisi kubaini walikuwa na mkono wa Albino huyo ambao walifukia ardhini mara baada ya kuukata.
Watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wa askari Polisi na kusomewa mashtaka yao huku wakitakiwa kutojibu lolote, ambapo upande wa Jamhuri ukiwashtaki kwa makosa mawili ikiwa ni pamoja na kosa la kula njama ya kutaka kuua na kujaribu kuua.
Miongoni mwa washtakiwa hao yupo Mume wa Albino huyo Gabriel Yohana, shemeji yake Gaudensi Yohana, Mganga wa jadi Kaponda Muyamba, Mtuhumiwa wa kutengeneza mchoro huo Linus Silukala na Mtuhumiwa aliyetaka kuununua mkono huo Mtogwa Cosmas alimaarufu kama mzee wa Ishu mkazi wa Sokomatola jijini Mbeya.
Hatahivyo mahakama hiyo iliyokuwa chini ya Hakimu mkazi Mh. Rosalia Mugisa imeweka wazi dhamana kwa watuhumiwa hao wote kwa pamoja huku mahakama hiyo ikitoa masharti manne ya dhamana hiyo, ikiwa ni pamoja na kuwa na wadhamini watatu wakazi wa wilayani Sumbawanga, fedha taslimu shilingi milioni tatu kila mmoja, na mmoja wa wadhamini awe ni mwajiriwa wa serikali au Shirika lolote la umma, ambapo washtakiwa hao walishindwa maaelekezo ya dhamana hiyo na kurudishwa mahabusu hadi Machi sita itakapotajwa tena.
Adolph Mbata, TBC Sumbawanga.
Last Updated ( Friday, 22 February 2013 11:23 )