Profesa Muhongo akemea malumbano ya kisiasa
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amekemea tabia ya baadhi ya watanzania kupoteza muda wao mwingi kwa kujadili mambo ya siasa, malumbano na kuongelea ya watu jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya Taifa.
Profesa Muhongo ameyasema hayo wakati akizungumza na wadau wa sekta ya nishati na madini mkoani Kilimanjaro na kusema kuwa dira ya maendeleo ya mwaka 2025 ni kuhakikisha tunakuwa na umeme wa uhakika na kuwa dira hiyo haitafikiwa iwapo watu wataendelea kupoteza muda kwa mambo yasiyo na msingi.
Wadau mbalimbali wa sekta ya nishati na madini mkoani Kilimanjaro wamekutana mjini Moshi na Waziri mwenye dhamana hiyo ili kujadili masuala mbalimbali ya uchumi na maendeleo yahusuyo sekta hiyo.
Akizungumzia suala la kuongeza uchumi na maendeleo, Profesa Muhongo amesema umefika wakati sasa kwa watanzania kupunguza siasa, malumbano na kuongelea ya watu badala yake kuzungumzia uchumi na maendeleo yaTaifa.
Pia amesisitiza kuwa ni vyema madiwani wakahakikisha kuwa shule za sekondari za kata zinapata umeme ili kusaidia wanafunzi kutumia teknolojia ya kisasa kwa kuangalia video za masomo mbalimbali ili kuleta maendeleo.
Sauda Shimbo, TBC Moshi.
Last Updated ( Wednesday, 19 September 2012 12:49 )